Jukwaa la Wananchi
Register Calendar
 
 
 


Reply
  Author   Comment  
Mkazi
Reply with quote  #1 
18th October 2011

Vijana wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wa Wilaya ya Monduli na wa kutoka mkoani Arusha, waliandamana jana hadi Kituo Kikuu cha Polisi jijini Arusha kumsindikiza Mwenyekiti wao wa mkoa, James Ole Millya, ambaye alitakiwa kujisalimisha kwa Jeshi la Polisi na kuthibitisha kauli yake aliyoitoa kwenye mkutano wa uzinduzi wa matawi ya CCM mkoani humo.

Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Akili Mpwapwa, wiki iliyopita alimtaka Millya kujisalimisha polisi kwa lengo la kuthibitisha kauli yake kuwa Jeshi la Polisi lilishinikizwa na mtoto wa kigogo wa serikali kuzuia mkutano ulioandaliwa na UVCCM Arusha na viongozi wa umoja huo waliotoka Makao Makuu Dar es Salaam, akiwemo Kaimu Mwenyekiti, Beno Malisa.

Polisi walisema watamhoji Millya kwa kauli zake ili awathibitishie huyo mtoto wa kigogo aliyezuia mkutano huo ni nani na polisi aliyezuia mkutano huo usifanyike ni nani. Polisi walisema hawakuzuia mkutano huo bali Katibu wa UVCCM Mkoa, Abdallah Mpokwa, alilitaarifu jeshi la polisi kwa simu kuwa mkutano huo umeahirishwa.

Hata hivyo, alisema Oktoba 10 vijana hao waliandamana bila kibali kwa maelezo walikuwa wanafungua matawi ya wakereketwa huku wakitoa kauli za kutuhumu Polisi kuwa wanazuia mkutano wao kutokana na shinikizo kutoka kwa mtoto wa kigogo wa serikali ambaye aliamuru mkutano huo usifanyike.

Millya hakuitikia wito wa kujisalimisha hadi alipokwenda jana akisindikizwa na vijana wenzake wakiwemo wa Wilaya ya Monduli walioongozwa na Mwenyekiti wao, Julius Kalanga.

Viongozi wa UVCCM mkoani Arusha walioambatana na Millya jana ni Katibu, Abdallah Mpokwa.

Vijana hao waliandamana jana saa 5:00 asubuhi kuanzia Makao Makuu ya UVCCM hadi Makao Makuu ya Polisi huku wakiwa katika makundi wakisema walikwenda kumsindikiza Millya ili kujua kama atahojiwa au la.

Baada ya kufika kituo cha Polisi, vijana hao walikaa pembeni wakimsubiri Millya awasili na ilipotimu saa 12:00 mchana Millya aliwasili akiwa na wakili wake, Moses Mahunda, na kusindikizwa na gari lingine lililokuwa na wazee.

Alipofika polisi vijana walikusanyika, lakini waliamuriwa na polisi waliokuwa maeneo hayo kutawanyika kwani eneo hilo ni dogo na vijana hao walitii amri hiyo na kwenda kumsubiri nje.

Baadaye Millya na Mahunda pamoja na baadhi ya viongozi wa UVCCM na wazee walikwenda ofisi ya Kamanda Mpwapwa ili kuitikia amri ya kujisalimisha.

Hata hivyo, walipofika ofisini kwake, Kamanda Mpwapwa alimuelekeza Millya aende leo kwa kuwa jana kulikuwa na shughuli za kupokea mwenge wa uhuru.

“Naomba uje kesho asubuhi maana leo kuna shughuli za mwenge hivyo hatutaweza kufanya mahojiano,” alisema Kamanda Mpwapwa.

Baada ya kuelezwa hivyo, Millya na kundi la vijana wa UVCCM walitoka wakitembea kwa miguu hadi ofisi za UVCCM Mkoa na kuzungumza na waandishi wa habari.

Millya alisema kuwa hadi sasa haelewi sababu za polisi kumuita kwa ajili ya mahojiano. “Polisi ni sehemu salama na mtu yeyote anaweza kuitwa na kuhojiwa hivyo nasubiri nijue naitiwa nini kwa kuwa mpaka sasa sijui naitwa kuhojiwa kwa sababu gani hivyo wacha nisubiri nione,” alisema Millya.

Wakati Millya akizungumza na waandishi wa habari, ofisi ya jengo la UVCCM ilikuwa imefungwa na kuwafanya vijana waliokusanyika hapo kuhoji ni kwa nini Mwenyekiti huyo azungumze nje ya ofisi tena ikiwa imefungwa wakati ni ofisi yake.

Vijana hao walisema kuwa Mwenyekiti wao alipaswa kuzungumza mambo ya chana akiwa ndani ya ofisi na kuongeza kuwa hayo ni mapambano na kuahidi kuwa watayashinda.

                               
                                        CHANZO:                                         NIPASHE                                
Previous Topic | Next Topic
Print
Reply


Create your own forum with Website Toolbox!