Jukwaa la Wananchi
Register Calendar
 
 
 


Reply
  Author   Comment  
Unregistered
Reply with quote  #1 


JAJI wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Aloyce Mujulizi, amejitoa kusikiliza kesi ya kupinga ubunge wa Arusha Mjini inayomkabili Mbunge wa jimbo hilo, Godbless Lema (CHADEMA), ambaye alidai hana imani naye.

Mujulizi alijitoa jana baada ya wakili wa Lema, Method Kimomogoro, kudai kuwa mteja wake hana imani na jaji huyo kwani CHADEMA kiliwahi kuituhumu Kampuni ya Uwakili ya IMMA, ambayo jaji huyo alikuwa mmoja wa wamiliki wake kuhusika na ufisadi uliotokea kwenye Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) kupitia Benki Kuu (BoT).

Akitoa uamuzi huo baada ya mvutano wa kisheria baina ya mawakili wa wadai na wadaiwa uliodumu kwa saa tatu, Jaji Mujilizi pamoja na uamuzi wake wa kujitoa alimuagiza Lema na Kimomogoro kuwasilisha ushahidi mahakamani hapo kuonyesha CHADEMA kiliwahi kuituhumu IMMA kuhusiana na ufisadi wa EPA .

Alisema kuwa endapo watashindwa kufanya hivyo ndani ya siku tano wachukue hatua za kikatiba za kuwasilisha rasmi maombi kwa rais ili aunde tume kuchunguza suala hilo ili ukweli uwekwe wazi, kwani kwa tuhuma zinazomkabili hastahili kushika nafasi ya ujaji.

Jaji Mujulizi alisema kuwa tume hiyo ya rais itasaidia kupatikana kwa ukweli juu ya suala hilo, hivyo kuepuka kuruhusu watu kuwatuhumu wengine mara kwa mara.

Alisema analirudisha jalada la kesi hiyo kwa Jaji Mfawidhi ili liweze kupangiwa jaji mwingine ambaye upande wa mlalamikiwa utakuwa na imani naye.

Awali jaji huyo alisema alipofika ofisini kwake alikuta taarifa kutoka kwa wakili Kimomogoro ikimweleza kuwa wanaendelea na msimamo wao wa awali wa kumtaka ajitoe kwenye shauri hilo kwa hoja kuwa haaminiki, hapaswi kuaminika kwa Lema na kwa CHADEMA.

“Wanadai CHADEMA kiliituhumu Kampuni ya IMMA Advocate niliyoifanyia kazi kabla ya kuteuliwa kuwa jaji kuwa ilikisaidia Chama cha Mapinduzi (CCM) kukwapua mamilioni ya fedha BoT ambazo zilitumika kukisaidia CCM kuingia madarakani mwaka 2005,” alisema.

Wakili wa watoa hoja, Alute Mungway alipinga taarifa hizo kwa kuwasilisha mahakamani hapo pingamizi mbili kuwa maombi hayo yalichelewa kuwasilishwa mahakamani hapo, jambo litakalochelewesha kumalizika kwa shauri hilo.

“Taarifa hiyo ilitakiwa iambatanishwe na hati ya kiapo pamoja na vielelezo lakini wao wametanguliza onyo kwamba ajitoe vinginevo wataleta ushahidi, hii ni kukutisha kama haujitoi tutaweka hadharani maovu yako au ya Kampuni yako ya IMMA advocate….haya walipaswa kuyaibua siku kesi hii ilipofika mbele yako kwa mara ya kwanza Julai, 8 mwaka 2011, si sasa,” alisema Mungway.

Alidai kuwa taarifa hiyo inakiuka mamlaka na taratibu za mahakama kwani ilileta mambo aliyodai kuwa ni ya uzandiki yenye kufedhehesha ambayo hayahusiani kabisa na shauri lililoko mahakamani ambalo jaji huyo anatakiwa kulitolea uamuzi huku likimfanya jaji hiyo kuacha jukumu la kusikiliza kesi ili afanye kazi ya kujitetea.

Wakili huyo alisema kuwa kwa mujibu wa taarifa hiyo upande wa walalakimikiwa wanaonyesha kuwa jaji na kampuni yake ni mafisadi ambao walipaswa kuwa magereza tangu mwaka 2005.

Alidai wakili Kimomogoro hakutimiza wajibu wake wa kuhakikisha analinda hadhi na mamlaka ya mahakama na watendaji wake kwa kile alichodai kuwa mambo aliyoleta mahakamani hapo ni mazito na yalipaswa kujadiliwa kwenye mahakama ya ndani na kufikiwa uamuzi kabla ya kuletwa kwenye mahakama ya wazi kama alivyofanya.

Hoja hiyo ilimfanya Jaji Mujulizi kuingilia na kusema kuwa wanasiasa wameanza kuvuka mipaka huku akimnukuu Mwanasheria wa Serikali, Jaji Frederick Werema aliyedai kuwa alisema bungeni kuwa: “Sijavuliwa ujaji kama michezo yenu ya siasa ni hii narudi mahakamani kuvaa joho niendelee na kazi yangu.”

Akijibu hoja hizo, wakili wa Lema, Kimomogoro alisema kuwa alipeleka taarifa hiyo kwa lengo la kutekeleza amri ya mahakama aliyoitoa jaji huyo wakati akiahirisha kesi hiyo Novemba 16 , mwaka jana ambapo aliwataka kueleza endapo wanaendelea na msimamo wao wa kumtaka ajitoe kusikiliza shauri hilo.

Wakili huyo alimhoji wakili Mungway kuwa anamtetea nani huku akisisitiza kuwa mteja wake na chama chake hawana imani na jaji huyo kutokana na kauli ya Katibu wa Itikadi na uenezi wa CCM, Nape Nnauye, kusema kuwa wana uhakika wa kushinda kesi hiyo.

Wakili huyo alisema kuwa baada ya Mhariri wa gazeti la Nipashe Jumapili, Florah Wingia, kutoa ushahidi mahakamani hapo kudai kuwa walimnukuu vibaya msemaji huyo wa CCM walipata uthibitisho wa sauti na picha vinavyomuonyesha Nape akitoa kauli hiyo.

“Kwanza Nape hakuja mahakamani aliogopa na yule mama (Florah Wingia) alisema uongo, nina CD inayothibitisha Nape kutoa kauli hizo na ni kati ya ushahidi tuliopanga kuwasilisha kujenga hoja ya kumtaka jaji ajitoe,” alisisitiza wakili huyo.

Alisema kuwa yupo tayari kuwasilisha mahakamani hapo ushahidi wa kumbukumbu rasmi za Bunge wakati CHADEMA wakiituhumu Kampuni ya IMMA kuhusika na ufisadi ambapo alihoji sababu za wakili Mungway kumtaka yeye na mteja wake kwenda polisi kutoa taarifa wakati suala hilo lilishaundiwa tume na rais.

Alisema kuwa kwenye tume hiyo iliyowashirikisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) na Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (PCCB) ambao baada ya uchunguzi walipeleka taarifa kwa rais ambaye aliamuru kampuni zilizohusika zirudishe fedha hizo vinginevyo zitafikishwa mahakamani.

Kesi hiyo ya uchaguzi namba 13 ya mwaka 2010 imefunguliwa mahakamani hapo na wananchi watatu ambao wote ni wanachama wa CCM, Mussa Mkanga, Happy Kivuyo na Agnes Mollel.

Source: T/daima 7 Feb 2012
Unregistered
Reply with quote  #2 
Inatia shaka sana iwapo uadilifu wa jaji unahojiwa. Mfumo wa kuwapata majaji wa Tanzania unatakiwa kupitiwa upya ili kuhakiisha wanakuwa confirmed na mhimili fulani ili kutunza heshima ya nafasi hii.
Previous Topic | Next Topic
Print
Reply


Create your own forum with Website Toolbox!