Jukwaa la Wananchi
Register Calendar
 
 
 


Reply
  Author   Comment  
Mkazi
Reply with quote  #1 


RAIS Jakaya Kikwete anapita katika moja ya vipindi vigumu katika utawala wake tangu alipoingia madarakani kwa mara ya kwanza zaidi ya miaka sita iliyopita, Tanzania Daima Jumatano linaweza kueleza kwa uhakika.

Misukosuko ya kisiasa, kiuchumi na kijamii inayolikabili taifa katika siku za hivi karibuni inayohusisha matukio kama yale ya mgomo sugu wa madaktari, kuzorota kwa uchumi, mvutano wa posho za wabunge na mjadala mkali wa Katiba, yote inaonekana kuelekezwa moja kwa moja kwa serikali anayoiongoza Kikwete.

Ukimya wa Rais Kikwete katika kuzungumzia tatizo la kuzorota kwa uchumi, mgomo wa madaktari ambao sasa umefikia hatua ya kuwahusisha madaktari bingwa na lile la kupanda kwa kiwango cha posho za wabunge umeibua minong’ono mingi kutoka kwa wadadisi mbalimbali wa mambo.

Hatua ya Rais Kikwete mwenyewe kutamka kwamba alikuwa hajapanga kuzungumzia masuala ya posho za wabunge na lile la mzozo wa madaktari wakati alipohutubia mjini Mwanza kwenye maadhimisho ya miaka 35 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni ushahidi kwamba taarifa za kuwapo kwa minong’ono hiyo kuhusu ukimya wake zimeshamfikia hata yeye mwenyewe.

Mbali ya wadadisi wa mambo kuhoji kuhusu ukimya huo wa rais, jingine linalojadiliwa ndani ya CCM na nje ya chama hicho ni kuendelea kubakia ofisini kwa waziri na naibu waziri wa Afya pamoja na watendaji wengine wa juu wa wizara hiyo ambao takriban wote wanaonekana kushindwa kuchukua hatua stahili za kuumaliza mzozo huo.

Habari ambazo Tanzania Daima Jumatano imezipata kutoka ndani ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii inayoendelea kuchunguza kiini cha mgomo huo wa madaktari zinaeleza kwamba kumekuwa na hoja nyingi zinazoelekeza katika kuwataka viongozi na watendaji wakuu wa Afya ambao takriban wote ni wateule wa rais kuwajibika.

Mgomo wa madaktari

Kama hiyo haitoshi, hatua yake ya kusafiri kwenda Davos nchini Uswisi na baadaye Addis Ababa, Ethiopia alikohudhuria mkutano wa wakuu wa Umoja wa Afrika wakati mgomo wa madaktari ukiendelea sambamba na kuzorota kwa uchumi nako kumezusha maswali mengi kuhusu namna rais anavyoyapa uzito matukio hayo mawili makubwa.

Baadhi ya wadadisi wa mambo wanauchukulia ukimya wa rais katika kulishughulikia suala zima la mzozo wa madaktari kuwa moja ya mambo ambayo yamechagiza kwa kiwango kikubwa kuendelea kukomaa kwa tatizo hilo ambalo tangu juzi limechukua taswira mpya baada ya madaktari bingwa kujiunga katika kadhia hiyo.

Mjadala wa Katiba ndani ya Bunge

Wakati tatizo hilo likiendelea kujisukasuka, Rais Kikwete anaonekana kukabiliwa na changamoto nyingine nzito ndani ya Bunge na hususan kutoka kwa baadhi ya wabunge wanaotokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao wanaonekana kukasirishwa na hatua zake mbili; mosi ikiwa ni ile ya kuzima ongezeko la posho za wabunge na la pili ikiwa ni hatua yake ya kukutana na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Licha ya Rais Kikwete, kujaribu kuwapoza wabunge wa CCM, waliopanga kukwamisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Katiba ya mwaka 2011, hoja hiyo inaonekana bado kuibua mpasuko miongoni mwa wabunge hao, huku wengi wakisisitiza kutobadili msimamo.

Katika kujaribu kupunguza makali ya mpasuko huo unaoweza kuiweka serikali ya Kikwete katika wakati mgumu kwenye mjadala unaotarajiwa kuanza leo, Waziri Mkuu Mizengo Pinda jana alikuwa akitarajiwa kukutana na wabunge wa CCM ili kupoza hasira za baadhi yao.

Pinda anaitisha kikao hicho ikiwa ni siku moja tu baada ya Rais Kikwete mwenyewe kukutana na kamati ndogo ya wabunge wa CCM ambayo imepewa kazi ya kuwashawishi wenzao kukubaliana na muswada huo.

Kamati hiyo ya wabunge wa CCM waliokutana na Kikwete inawajumuisha, Jenister Mhagama (Peramiho), Christopher Ole Sendeka (Simanjiro), Peter Serukamba (Kigoma Mjini), Balozi Seif Ali Idd (Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Zanzibar) na Mohamed Ali Chombo (Magomeni, Zanzibar).

Katika mkutano huo wa Pinda, wabunge wa CCM walikuwa wakitarajiwa kupokea taarifa na msimamo wa Rais Kikwete dhidi ya tishio la wabunge walioapa kuukwamisha muswada huo kwa madai kuwa sheria hiyo ambayo tayari ilishasainiwa, ilifanyiwa marekebisho ya baada ya Kikwete kukutana na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Chama cha Wananchi na NCCR-Mageuzi, Ikulu jijini Dar es Salaam.

Miongoni mwa hoja ambazo zinatajwa kuwa zitatumika kuwapooza wabunge hao wa CCM ni ile ya kuwataka kuachana na mawazo kwamba mabadiliko hayo yanatokana na ushawishi wa CHADEMA bali ni matokeo ya vikao vya rais na wadau mbalimbali, kikiwamo hata CCM ambayo nayo iliwasilisha mapendekezo yake nane ya marekebisho.

Wakati kukiwa na matumaini hayo, baadhi ya wabunge waliozungumza na Tanzania Daima Jumatano wameendelea kushikilia msimamo wao wa kupinga mapendekezo yoyote ya marekebisho ya sheria hiyo ya Katiba.

Mmoja wabunge wenye mawazo hayo ni Ali Mohamed Kessy (Nkasi) ambaye aliielezea hatua yoyote ya kupitisha marekebisho hayo kuwa ni sawa na ya kula tena matapishi, jambo ambalo alisema yeye binafsi hakubaliani nalo.

“Tulishakubaliana kwamba hatutapitisha muswada huo hata kama rais atafikia uamuzi wa kuvunja Bunge, ni sawa tu, lakini hatuwezi kula matapishi yetu,” alisema Kessy.

Mbunge mwingine mwenye mawazo ya namna hiyo ni Godfrey Zambi (Mbozi Mashariki), ambaye ni juzi tu alikaririwa na kituo cha Televisheni ya Taifa (TBC), akisisitiza msimamo wa kutokuwa tayari kupitisha muswada huo.

Hata hivyo, wakati wabunge hao wakiendelea kushikilia msimamo huo, mbunge mwingine wa CCM, Livingstone Lusinde (Mtera), ambaye aliingia bungeni baada ya kumwangusha mzee John Malecela, katika hatua ya kura za maoni ndani ya chama hicho, alilieleza gazeti hili kwamba binafsi hana ubavu wa kushindana na Rais Kikwete.

“Mimi nawashangaa wabunge wanaosema watakwamisha muswada huo kwa madai kuwa rais kaingiza mapendekezo ya CHADEMA. Binafsi sioni tatizo kwani sina ubavu wa kushindana naye,” alisema Lusinde ambaye amepata kuwa mwanachama wa chama hicho cha upinzani kabla ya kujiunga na CCM baadaye.

Katika marekebisho yaliyopewa jina la Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 Na. 8 ya mwaka 2012, serikali imeridhia vyama vya siasa, asasi za kiraia, vyama vya kitaaluma na asasi za kidini kuteua wajumbe wa kuingia kwenye Tume ya Katiba.

Serikali imekubali kufanya mabadiliko katika kifungu cha 6 (1) cha sheria hiyo kwa kuondoa mamlaka ya uteuzi moja kwa moja kwa rais.

Kifungu cha 6 (1) cha sheria, sasa kinasema rais atateua wajumbe kutoka miongoni mwa majina atakayopelekewa na vyama vya siasa, asasi za kiraia, taasisi za kidini na vyama vya kitaaluma kuwa wajumbe wa Tume ya Katiba.

Aidha, serikali imeridhia matakwa ya CHADEMA ya kuongeza kifungu cha 17 (10), kinachoruhusu watu binafsi, taasisi za kidini na vyama vya hiari kutoa elimu ya uraia. Asasi hizo sasa zitakuwa zinaripoti kwa mkurugenzi wa halmashauri badala ya mkuu wa wilaya.

Vile vile serikali imeridhia kufutwa kwa kifungu ch 6 (5) (c) kilichokuwa kinawaondolea sifa wajumbe wa tume, watu waliowahi kuhukumiwa kwa kutenda kosa au mtuhumiwa katika shauri lililoko mahakamani linalohusu shitaka la kukosa uaminifu au maadili.

Ibara nyingine ambayo imefanyiwa marekebisho kwa mujibu wa makubaliano kati ya Rais Kikwete na CHADEMA ni 6 (5) (a) ambapo madiwani au viongozi wa vyama vya siasa wa ngazi zote waliokuwa wamezuiliwa kuwa wajumbe wa tume, sasa wameruhisiwa.

Jingine ambalo CHADEMA walipendekeza na serikali kuridhia ni kuhusu kuwapo kwa kamati ya nidhamu ya tume ya Katiba.

Awali, sheria hiyo ilikuwa kimya kuhusu kamati ya nidhamu, lakini sasa kimeongezwa na kitakuwa kinaongozwa na mtu mwenye hadhi ya ujaji wa Mahakama ya Rufaa, akishirikiana na wajumbe wanne kutoka Tume ya Haki za Binadamu, Utawala Bora, Tume ya Maadili ya Umma, Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) na Chama cha Wanasheria Zanzibar (ZLS).

Posho za wabunge

Habari zaidi kutoka miongoni mwa wabunge wa CCM zinaeleza kwamba, sababu nyingine inayowachochea kufikiria kuyakwamisha marekebisho hayo ni hatua ya rais kupiga danadana suala la ongezeko la posho za wabunge hata kusababisha kuibuka kwa mvutano kati ya Ikulu kwa upande mmoja na Waziri Mkuu Pinda na Spika Anne Makinda kwa upande mwingine.

Hatua hii imefikiwa baada ya Ikulu kutoa tamko linaloeleza kwamba, rais hakusaini sheria ya ongezeko la posho za wabunge ambalo kimsingi lilikuwa likipingana na kauli zilizotolewa na Pinda na Makinda, ambapo wote walikaririwa wakisema rais alikuwa amesaini sheria hiyo.

Source: T/daima
Previous Topic | Next Topic
Print
Reply


Create your own forum with Website Toolbox!