Jukwaa la Wananchi
Register Calendar
 
 
 


Reply
  Author   Comment  
Mkazi
Reply with quote  #1 
18th October 2011
  Ahamishia moto wa bungeni baraza la madiwani
  Wamwacha mwenyekiti na maumivu, watoka nje
  Mbunge CCM aliyetelekezwa aalikwa Chadema
                                               

                                               
Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu (wa pili kulia) akizungumza na waandishi wa habari baada ya wabunge wa chama hicho kususia kikao cha Baraza la Madiwani mkoani Singida jana.
                                       

Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, amewaongoza madiwani wa chama chake kutoka nje ya kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Singida, baada ya kubaini kuwa kanuni za kuitisha kikao hicho zilikiukwa.

Lissu ambaye ni diwani wa halmashauri hiyo, aliwaongoza wenzake watatu kususia kikao hicho, baada ya kuafikiana nao kwamba walipelekewa makabrasha yenye nyaraka za kikao hicho siku moja kabla ya kikao, jambo ambalo ni kinyume cha taratibu.

Kwa mujibu wa kanuni za kudumu za uendeshaji wa vikao vya baraza la madiwani, makabrasha hayo ambayo yana nyaraka mbalimbali zikiwemo ajenda za kujadiliwa, yanatakiwa kuwafikia wajumbe (madiwani) siku saba kabla ya kikao.

Kufuatia hali hiyo, madiwani hao wa Chadema walilalamikia kuchelewa kupelekewa makabrasha hayo.

Diwani wa Kata ya Isseke, Amosi Mghenyi, alisema kuchelewa kupelekewa makabrasha ni ukiukwaji wa kanuni za halmashauri hiyo inayotaka diwani apewe kabrasha la kikao siku saba kabla ya kikao, na kuungwa mkono na wenzake watatu.

Baada ya Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Celestin Yunde, kufungua kikao hicho, Mghenyi aliinua mkono akisema ana ombi maalum.

Aliporuhusiwa alikieleza kikao kuwa baadhi ya madiwani walipata makabrasha juzi (Jumapili) wakati kanuni inataka wayapate siku saba kabla ya kikao.

Alisema kutokana na hali hiyo anaomba kikao hicho kiahirishwe hadi baada ya siku saba ili madiwani wote wapate muda wa kuyasoma na kuyaelewa vizuri makabrasha hayo.

Baada ya hatua hiyo, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Hinga Mnyawi, alisema jiografia ya halmashauri hiyo hairuhusu madiwani wote kupelekewa makabrasha na kwamba ni gharama kubwa ambayo bajeti ya halmashauri hairuhusu.

Mnyawi ambaye ni Diwani wa CCM Kata ya Ikhanoda, alisema badala yake kupitia vikao halali, waliamua kwa kauli moja makabrasha yawe yanapelekwa katika ofisi za vyama vya siasa ili kuepuka gharama kubwa.

Baada ya kauli hiyo, Lissu, alisimama na kukiomba kikao hicho kikubaliane na mambo mawili na yawekwe kwenye kumbukumbu za kudumu za halmashauri hiyo.

Lissu alitaja mambo hayo kuwa ni kikao kikubaliane kuvunja kanuni iliyojiwekea ya madiwani kupewa makabrasha siku saba kabla ya kikao ili mambo yawe yanafanywa kiholela holela.

“Jambo la pili ni kikao endapo kitatambua kuwa kuvunja kanuni ni dhambi, basi kikao kiahirishwe ili madiwani wakasome makabrasha kwa kipindi cha siku saba na baada ya siku hizo, kikao kiitishwe,” alisema. Hata hivyo, Mwenyekiti Yunde aliingilia kati na kutaka malumbano yaepushwe ili kutopoteza muda. Badala yake aliwataka wanaotaka kikao kiendelee wanyooshe mikono juu. Zaidi ya robo tatu ya madiwani walinyanyua mikono juu na mwenyekiti huyo aliruhusu kikao kiendelee.

Uamuzi huo ulimfanya Lissu aliyekuwa amekaa mbele, kunyanyuka na kukusanya makabrasha yake yote na kuanza safari ya kutoka nje ya ukumbi wa mikutano huku madiwani wa CCM wakimpigia makofi kwa nguvu. Madiwani wengine watatu wa Chadema nao walinyanyuka na kumfuata Lissu nje ya ukumbi.

Akizungumza na waandishi wa habari nje ya ukumbi kuhusiana na uamuzi huo, Lissu, alisema madiwani 62 wa CCM wamezoea kuendesha vikao kwa mazoea kwa ajili ya kuficha ubadhirifu kwenye halmashauri.

“Sisi kwa kweli tumekataa na tutaendelea kukataa kuburuzwa, tunachokipigania ni kuhakikisha kanuni na sheria tunazojiwekea hazivunjwi kwa maslahi ya chama chochote cha siasa. Wachache wanataka kulinda maslahi yao,” alisema.

Alisema watapigania hali hiyo hadi utamaduni wa kuheshimu kanuni na taratibu za kuendesha vikao utakapofuatwa kwa maslahi ya wananchi wa wilaya hiyo.

Hata hivyo, akifunga kikao hicho, Mwenyekiti Yunde alitumia muda huo kuziagiza mamlaka zinazohusika kuhakikisha kwamba zinaandaa na kupeleka makabrasha kwa wahusika ndani ya siku saba kabla ya kikao ili waweze kuyapitia vizuri. Tukio la madiwani hao kususia kikao ni mwendelezo wa madiwani wa Chadema kutoka nje ya vikao vya halmashauri kupinga kuburuzwa na madiwani wa CCM.

Wiki iliyopita, madiwani wa chama hicho katika Jiji la Mbeya walitoka nje ya kikao wakidai kuwa hoja ambazo zilipaswa kuzungumzwa hazikuwa sehemu ya ajenda ya kikao hicho.

Mkakati wa kususia vikao kwa kutoka nje ulianzia bungeni mwaka jana baada ya wabunge wa Chadema kususia uzinduzi wa Bunge la 10 uliofanywa na Rais Jakaya Kikwete.

Kadhalika, wabunge hao walitoka tena nje ya Bunge wakipinga marekebisho ya kanuni za Bunge juu ya maana ya kambi rasmi ya upinzani.

MBUNGE WA MBARALI AKARIBISHWA CHADEMA

Katika hatua nyingine, Mbunge wa Mbarali CCM, Dickson Kilufi, ameshauriwa kukihama chama chake na kujiunga na Chadema ambacho kinatetea wananchi.

Ushauri huo ulitolewa na Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Mbeya Mjini, John Mwambigija, wakati akiwahutubia wananchi wa Rujewa katika wilaya ya Mbarali katika operesheni ya Chadema Twanga Kotekote. Alisema anamshauri Kilufi kuachana na CCM na kujiunga na chama hicho.

Alisema anamshauri hivyo kutokana na CCM kutokuwa na sera za kuwasaidia wananchi wa Rujewa kutatua matatizo yanayosababishwa na wawekezaji wanaoonyesha ubabe kwa wananchi wazawa. Alisema wakati Mbunge Kilufi alipokamatwa na polisi na kupelekwa jijini Mbeya na kufunguliwa kesi, hakuna kiongozi yeyote wa CCM aliyejitokeza kumsaidia hata kumwekea dhamana, hali iliyoonyesha kuwa hawamjali wala kumthamini.

Kutokana na hali hiyo, alimtaka Kilufi kujitoa CCM na kujiunga na Chadema na kumuhaidi kuwa akiwa Chadema atapata ubunge kwa kuwa wananchi wanampenda kutokana na utendaji wake mzuri wa kazi.

“Kilufi ni kipenzi cha wana-Mbarali kutokana na utendaji wake wa kazi anaouonyesha hata ukihama chama chako bado utapata nafasi huku kwani wananchi wanaangalia utendaji wako na sio chama,” alisema Mwambigija.

Alisema Kilufi ni mwanaharakati mpigania ardhi wana-Mbarali dhidi ya wawekezaji wanaotaka kuwageuza wananchi manamba wakati nchi iko huru.

Mwambigija alisema: “Kilufi anaimba kama malaika na anacheza kama shetani kwani anasaidia wananchi wakati chama hakina sera ya kusaidia wananchi.”

WANACCM WAJIUNGA CHADEMA

Wakati huo huo, zaidi ya wanachama 50 wa CCM, akiwemo aliyekuwa kada wa chama hicho wa kikosi cha Green Guard, Ayub Mlwilo, mkazi wa Rujewa na wakazi wengine 138 wamejiunga na Chadema.

Mavuno hayo ya Chadema yalitokana na mkutano mkubwa walioufanya juzi katika maeneo tofauti wilayani Mbarali, ambapo pamoja na mambo mengine, kukusanya changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi wa maeneo hayo.

Akiwapokea wanachama hao wapya, Mwambigija, aliwataka kusoma ilani ya chama hicho na kuielewa ili wasiwe watu wa kuhangaika kwenda vyama vingine vyenye ilani zisizotekelezeka.

“Sisi Chadema tunatekeleza yale ambayo tumeayaandika, tulisema tutakuwa tukiwashirikisha wananchi wetu kuhusu mambo mbalimbali yanayowahusu na kutaka ushauri kwao, ndicho tunachofanya leo,” alisema.

Aidha, Mwambigija, aliwaeleza wananchi kuwa inapotokea baadhi ya watu hasa walio ndani ya CCM kutetea maslahi ya wananchi huitwa wasaliti na kuundiwa kesi zisizokuwa na ukweli wakidaiwa kuwa wafuasi wa Chadema.

Alimtaka Mbunge Kilufi kuachana na siasa za kinafiki na kujiunga na Chadema ili aweze kutimiza ndoto zake za kuwatetea wananchi wake katika kuhakikisha wanapiga hatua ya kimaendeleo, ukiwemo umilikaji wa ardhi.

Baadhi ya wanachama waliojiunga na Chadema wakitokea CCM walisema waliamua kuihama CCM kutokana na kubaini njama na mazingira ya kutaka kumwangamiza mbunge wao ambaye wanaamini ndiye mtetezi wao.

                               
                                        CHANZO:                                         NIPASHE                                
Previous Topic | Next Topic
Print
Reply


Create your own forum with Website Toolbox!