Jukwaa la Wananchi
Register Calendar
 
 
 


Reply
  Author   Comment  
Unregistered
Reply with quote  #1 


VYAMA vya NCCR-Mageuzi na Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), baada ya mazungumzo ya muda mrefu, vimekubaliana kufuta kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi ya Jimbo la Kawe yaliyomtangaza Mbunge wa jimbo hilo, Halima Mdee (CHADEMA) kuwa mshindi.

Kesi hiyo ya kupinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu katika Jimbo la Kawe, ilifunguliwa Novemba 25, 2010 na aliyekuwa mgombea wa jimbo hilo kupitia NCCR-Mageuzi ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, James Mbatia.

Mbatia alifungua kesi hiyo dhidi ya Mdee, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Msimamizi wa Uchaguzi, akilalamika kuwa Mdee katika mikutano ya kampeni alimwita ni fataki anayefanya mapenzi na watoto wa shule, kibaraka wa CCM na kila wiki amekuwa akilipwa sh milioni 80 na CCM, hivyo kuwataka wapiga kura wa jimbo hilo wasimchague.

Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Makao Makuu ya NCCR-Mageuzi na kushirikisha maofisa waandamizi wa vyama hivyo akiwamo Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Samuel Ruhuza na mawakili wa pande zote, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, alisema kuwa uamuzi uliofanywa na vyama hivyo umezingatia masilahi ya wananchi na taifa kwa ujumla.

Alisema kimsingi baada ya kufunguliwa kwa kesi hiyo, vyama hivyo vimekuwa na mazungumzo ya karibu sana ili kuona uwezekano wa kuifuta kabisa.

Kwa mujibu wa Dk. Slaa, gharama za uchaguzi mdogo ni kubwa sana ambazo zinawaingizia hasara Watanzania, hivyo kwa kuepuka hali hiyo, wamelazimika kuifuta bila kuwapo kwa masharti yoyote.

“Kwa vile kuna gharama zilizotumika kwenye uendeshaji wa kesi hiyo, kila chama kitabeba mzigo huo. Tumeuanza mwaka huu kwa habari njema,” alisema na kuongeza kuwa, kwa vile NCCR-Mageuzi waliweka sh milioni tisa mahakamani wakati wa kufungua kesi hiyo, fedha hizo zitarejeshwa kwao.

Alisema katika uamuzi huo waliokubaliana, kimsingi kama kuna ushindi walioshinda ni wananchi wa Kawe kwani vyama hivyo vipo kwa ajili ya masilahi ya wananchi.

Dk. Slaa ambaye ndiye alikuwa mzungumzaji mkuu, alisema uhusiano wa vyama hivyo hautaishia kwenye tukio hilo tu, na kwamba vimekuwa na historia ndefu ya kushirikiana.

Kuhusu kusimamisha mgombea mmoja kwenye jimbo au urais, alisema mazungumzo yanaendelea na kuna uwezekano ikafika wakati wakamsimamia mgombea mmoja kulingana na mahitaji ya wakati.

Wakizungumzia kwa nyakati tofauti kuhusu masilahi ya wananchi wa Arusha ambao madiwani wao walifukuzwa kwenye chama na Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), makatibu hao wakuu walisema suala la viongozi hao ni la utovu wa nidhamu.

Walisema kila chama kina taratibu na kanuni zake, hivyo zinapovunjwa na viongozi wenyewe ni kukidhalilisha chama, hivyo hatua iliyofikiwa ya kuwafukuza uanachama ni kuimarisha misingi iliyoanzisha vyama hivyo.

Mbatia na Mdee wakiwa hawapo kwenye kikao hicho cha jana, Dk. Slaa alimtetea mbunge wake kuwa yuko kwenye mjadala mzito bungeni wakati Mbatia yuko kwenye kikao muhimu.

Kabla ya kufikiwa kwa uamuzi huo wa kufuta kesi, kesi hiyo jana ilikuwa isomwe maelezo ya awali na ingeanza kusikilizwa kwa mfululizo kuanzia leo hadi Ijumaa.

Mbatia katika kesi hiyo iliyokuwa mbele ya Jaji John Utamwa, alikuwa akiwakilishwa na wakili Mohamed Tibanyendera wakati Mdee alikuwa akiwakilishwa na wakili Mabere Marando na Edson Mbogoro.

Source: T/daima 7 Feb 2012
Previous Topic | Next Topic
Print
Reply


Create your own forum with Website Toolbox!