Jukwaa la Wananchi
Register Calendar
 
 
 


Reply
  Author   Comment  
mdau

Moderators
Registered:
Posts: 42
Reply with quote  #1 
KUFANYIKA KWA UCHAGUZI MDOGO WA UBUNGE KATIKA JIMBO LA ARUMERU MASHARIKI NA CHAGUZI NDOGO ZA MADIWANI KATIKA KATA ZA HALMASHAURI MBALIMBALI NCHINI

Tume ya Taifa ya Uchaguzi inapenda kuwatangazia wananchi wote kuwa, imepokea barua kutoka kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, yenye kuiarifu kuhusu kuwepo kwa nafasi wazi ya Kiti cha Ubunge katika Jimbo la Arumeru Mashariki kutokana na kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo Mhe. Jeremiah Solomon Sumari, aliyefariki dunia tarehe 19 Januari, 2012. Baada ya Tume kupokea taarifa hiyo ya kuwepo nafasi wazi kwa Jimbo la Arumeru Mashariki, Tume imepanga kufanya Uchaguzi Mdogo wa Ubunge katika Jimbo hilo kwa mujibu wa sheria ili kujaza nafasi hiyo ya Ubunge iliyoachwa wazi.

Ratiba ya kufanyika kwa Uchaguzi Mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Arumeru Mashariki ni kama ifuatavyo:-

NA         TUKIO         TAREHE
1.         Uteuzi wa Wagombea         08 Machi, 2012
2.         Kampeni za Uchaguzi         09 Machi, 2012 hadi 31 Machi, 2012
3.         Siku ya Upigaji Kura         01 Aprili, 2012

Aidha, Tume inapenda kuwataarifu wananchi kuwa itafanya Chaguzi Ndogo za Madiwani katika Kata nane (8) zilizoko katika Halmashauri mbalimbali nchini kufuatia kuwepo wazi kwa nafasi za Viti vya Madiwani ambazo zimetokana na vifo vya Madiwani husika.

Ratiba ya kufanyika kwa Chaguzi Ndogo hizo za Madiwani ni kama ifuatavyo:-

NA         TUKIO         TAREHE
1.         Uteuzi wa Wagombea         05 Machi, 2012
2.         Kampeni za Uchaguzi         06 Machi, 2012 hadi 31 Machi, 2012
3.         Siku ya Upigaji Kura         01 Aprili, 2012

Kata zitakazohusika katika Uchaguzi huo na Halmashauri zake ni kama ifuatavyo:-

NA         HALMASHAURI HUSIKA         KATA ITAKAYOFANYA UCHAGUZI
1.         Temeke         Vijibweni
2.         Bagamoyo         Kiwangwa
3.         Kirumba         Mwanza
4.         Bariadi         Logangabilili
5.         Dodoma         Chango’mbe
6.         Rungwe         Kiwira
7.         Songea         Lizaboni
8.         Tanga         Msambweni

Ifahamike kwamba, hakutakuwa na kuandikisha Wapiga Kura kwa ajili ya Chaguzi hizo. Daftari la Kudumu la Wapiga Kura lililotumika wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita ndilo litakalotumika katika Uchaguzi Mdogo wa Ubunge Jimbo la Arumeru Mashariki na Chaguzi zote Ndogo za Madiwani. Vituo vitakavyotumika kupiga kura ni vile vilivyotumika wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2010.

Tume itaweka orodha ya Wapiga Kura katika Vituo vya Kupigia Kura kwa muda wa siku saba (7) kuanzia tarehe 25/03/2012 hadi 31/03/2012. Wananchi wote wa Jimbo la Arumeru Mashariki na Kata zote ambazo Chaguzi Ndogo zitafanyika mnaombwa kwenda katika vituo vyenu vya Kupiga Kura na kukagua majina yenu ili kujua Vituo mtakavyo pigia Kura.

Tume inapenda kuwasisitizia wananchi na Vyama vyote vya Siasa kuzingatia na kufuata ratiba ya uchaguzi iliyotolewa na Tume na kujitokeza kwa wingi kushiriki katika mchakato mzima wa Uchaguzi kuanzia siku ya Uteuzi wa Wagombea, Kampeni za Uchaguzi, kukagua orodha ya Wapiga Kura wakati itakapobandikwa kwenye Vituo na kujitokeza kwa wingi siku ya upigaji kura tarehe 01 Aprili 2012. Vituo vya Kupiga Kura vitafunguliwa saa 1:00 asubuhi na kufungwa saa 10:00 alasiri.

Tume inawakumbusha wananchi wote katika maeneo husika kutunza vizuri Kadi zao za kupiga kura na kuzitumia siku ya upigaji Kura. Aidha, ikumbukwe kwamba kama Mpiga Kura hutakuwa na kadi ya Kupiga Kura hutaruhusiwa kupiga kura. Hakikisha unatumia haki yako ya kikatiba kushiriki katika Uchaguzi na kuchagua viongozi unaowataka.


Damian Lubuva
MWENYEKITI
TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI
Previous Topic | Next Topic
Print
Reply


Create your own forum with Website Toolbox!